Dodoma. Wabunge wa CCM jana mchana walimgomea
Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge (Party Cocas) ya chama hicho, Mizengo
Pinda na kushinikiza mawaziri watatu ambao wizara zao zimetajwa
kushindwa kusimamia vyema Operesheni Tokomeza Ujangili wajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa
mawaziri walioshinikizwa kujiuzulu wenyewe ni pamoja na Balozi Khamisi
Kagasheki ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Emmanuel Nchimbi
(Waziri wa Mambo ya Ndani) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Pius
Msekwa bungeni jana kiliitishwa na Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu kwa
lengo lililoelezwa ni kuwapoza wabunge.
Chanzo cha habari kutoka katika kikao hicho
kilisema kuwa wabunge hao walitaka mawaziri hao kujiuzulu wenyewe ili
kukinusuru chama mbele ya wananchi.
“Tumemtaka Waziri Mkuu akakae na wenzake na
kutuambia kama wanajiuzulu au la na kutupa jibu kabla ya kuahirishwa kwa
Bunge, mtasikia wenyewe baadaye ndani ya Bunge,”kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa kikao hicho na
wabunge kurejea bungeni, Pinda hakurejea bungeni, badala yake ilidaiwa
kwamba alikuwa na kikao katika ofisi zake zilizopo bungeni.
Hadi saa 11.25 alasiri wakati kikao cha Bunge
kikiendelea Waziri Mkuu alikuwa hajarejea bungeni, huku ikielezwa kwamba
katika kikao alichokuwepo hakikuwahusisha mawaziri wanne waliokuwa
katika shinikizo la kujiuzulu.
chanzo MWANANCHI
chanzo MWANANCHI

0 maoni:
Chapisha Maoni