Huu ni ukatili ambao wanafanyiwa wajawazito si kule Rukwa pekee, bali nchini kwa jumla
Sumbawanga. Siyo jambo geni kusikia wanawake wakiwalalamikia wauguzi ama kwa kuwapiga au kuwatukana wakati wa kujifungua.
Hata hivyo, matukio ya mama kupoteza maisha ama
mtoto aliye tumboni kufariki kwa ajili ya vitendo hivyo vimekuwepo,
lakini siyo kwa wingi.
Rehema Michael (18), mkazi wa Kijiji cha Tentula
Sumbawanga Vijijini ni mmoja kati ya waliokutana na chungu ya kutukanwa
na kupigwa na muuguzi wakati wa kujifungua.
Rehema ambaye ilikuwa ni mimba yake ya kwanza, amepoteza mtoto na yeye mwenyewe kunusurika kifo kutokana na hali yake.
Rehema akiwa mchovu anasimulia kwa uchungu kisa chote tangu alipopata uchungu wa kujifungua mpaka alipofikishwa hospitali.
“Nilisikia uchungu siku ya Jumatatu, nikamwambia mama mkwe ,tukaondoka naye kwenda kwenye zahanati ya pale kijijini Tentula.
“Tulipofika hatukumkuta muuguzi wa zamu na daktari
tuliyemkuta hakuwa na funguo ya chumba kwa hiyo akatubeba kwenye
pikipiki mpaka kwenye kituo cha afya cha Ikozi.
“Nilipofika hapo nikaingizwa kwenye chumba cha
kuzalia, nikawa najitahidi kusukuma mtoto, nesi akanipiga ili nisukume
mtoto, nilijitahidi kusukuma mtoto mpaka kichwa kikaanza kutoka hadi
kufikia kidevu, lakini kwa kuwa nilivyokuwa napigwa nikaishiwa nguvu.
Muuguzi akaniambia niache uvivu, “Sukuma, acha
ujinga, nani alikutuma?” akaendelea hivyohivyo, kwa kweli nilikuwa
nasikia maumivu sana.
Nilipoishiwa nguvu aliendelea kunipiga ili
nisukume mtoto, lakini nikashindwa ndiyo ikabidi gari liitwe ili niletwe
hapa kwenye hospitali ya mkoa.
Nilifika huko mtoto akining’inia, hivyo mpaka
ninafika hapo, nilipotoka huko mpaka mtoto alikuwa hai, lakini mpaka
nafikikishwa hapo, nikaambiwa mtoto ameshakufa.
Nilipofika hapo nesi akanichoma sindano na kumtoa mtoto kirahisi, lakini ndiyo akawa ameshakufa, na mimi nilikuwa nimechoka.
Kilichonifanya niishiwe nguvu ni kwa sababu ya kupigwa, kama mtu anajitahidi kusukuma mtoto mimi sioni ni kwa nini apigwe.
Gari kutoka katika eneo hilo mpaka Sumbawanga mjini ni mwendo wa kama saa mbili.”
Anasema alifika hospitalini hapo akiwa amechoka, madaktari wakamchoma sindano na kumtoa mtoto huku tayari akiwa ameshafariki.
Wataalamu wa afya kwa upande wao wanasema kuwa,
mimba ya kwanza ni moja ya kiashiria cha hatari kwa mama mjamzito hivyo
wauguzi hutakiwa kumshauri mama huyo kuhakikisha anajifungulia kwenye
hospitali kubwa.
Rehema anasema kuwa, licha ya kwamba alikuwa
anahudhuria kliniki siku zote hakuwahi kuambiwa kwamba anatakiwa
kujifungulia kwenye hospitali kubwa.
Naye Grace Kamungwi (27), kutoka Mtowisa, pia
katika Manispaa ya Sumbawaga alipoteza mtoto naye kunusurika kifo
kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni uzembe wa wauguzi.
Akisimulia kilichomkuta, anasema: “Nilipata
uchungu, Jumatatu nikaenda Kituo cha Afya cha Mtowisa, nilipofika huko
nilijitahidi sana kusukuma mtoto atoke, lakini nikashindwa.
Nikaletwa hapa hospitali ya mkoa, baada ya
kunifanyia upasuaji wakaniambia mtoto tayari amefariki. Hii ni mimba
yangu ya kwanza na ya pili nilijifungua kawaida kabisa bila kupata
tatizo lolote.
Mtoto wangu wa kwanza ana miaka mitano, wa pili nilijifungua mwaka 2012, akafariki.
Dk Francis Mashi aliyekuwa akimuhudumia Grace
katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Rukwa anasema kuwa mama huyo alipata
uchungu mkingamo na ilikuwa lazima afanyiwe upasuaji.
“Huyu alikuwa kwenye uchungu kwa muda mrefu, mtoto
alikuwa amekaa vibaya na asingeweza kujifungua kwa njia za kawaida.
Ukiwa na uchungu mkingamo, huwezi kujifungua kwa njia ya kawaida na
inatakiwa uambiwe mapema ili ujifungulie kwenye hospitali inayoweza
kufanya upasuaji.”
Kituo cha Afya Mtowisha kinatakiwa kifanye upasuaji lakini kuna wakati huwa wanashindwa.
Anasema Dk Mashi kuwa mtoto aliyekaa vibaya,
ilitakiwa alipokuwa akihudhuria kiliniki suala hilo litambuliwe na
atakiwe kwenda kujifungulia kwenye hospitali kubwa inayoweza kufanya
upasuaji
Chanzo: Mwananchi

0 maoni:
Chapisha Maoni