Dodoma. Taasisi isiyokuwa ya kiserikali
ya Mwalimu Nyerere Idealogy Conservation Society ya jijini Tanga,
imefungua Kesi Mahakama Kuu ikitaka kuzuia mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba.
Taasisi hiyo inapinga mchakato huo wa Katiba kwa
kile inachodai kuwa ni kasoro zilizojitokeza, ikiwamo wananchi kukosa
uwakilishi uliotokana na ridhaa yao, posho kubwa wanayolipwa wajumbe na
gharama kubwa zilizotumika katika maandalizi ya Bunge hilo.
Kesi hiyo ya madai namba 02/2014, ilifunguliwa
Februari 17, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga na mwenyekiti
wa taasisi hiyo, Dk. Muzzammil Mussa Kalokola.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa kwa
stakabadhi ya malipo ya Serikali namba 49803745, ni Waziri wa Sheria na
Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), (kwa sasa ni Frederick
Werema) na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji
Mstaafu, Joseph Warioba.
Hata hivyo Jaji Werema na Jaji Warioba wamesema hawana taarifa za kesi hiyo.
Dk. Kalokola alisema katika hati yake ya madai kuwa anataka mchakato huo wa Katiba usitishwe kwa kuwa umevunja Katiba iliyopo.
Amesema Katiba ya sasa imekiukwa katika Muundo wa
Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika utekelezaji wa
majukumu na wajibu wake wa kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya
Madadiliko ya Katiba ibara ya 98.
“Vilevile imeshindwa kuzingatia hadidu za rejea
kama zilivyoainishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83,”
alisema Dk Kalokola.
Dk. Kalokola alifafanua kuwa Katiba ya sasa
imeweka masharti kadhaa, ikiwamo utaratibu wa namna ya kuibadilisha na
sheria nyingine ambazo zimeanishwa katika ibara ya 98 na Sheria ya mwaka
1984 Na.15 ib.14.
“Ibara ya 98 (1) Bunge laweza kutunga sheria kwa
ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni
zifuatazo,” alisema huku akiinukuu ibara hiyo na kuendelea:
“Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha
masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b)
ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa
katika orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura
za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote.
“Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha
masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote
yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya
Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni mwa Katiba hii,
utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao
haipungui theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Bara na
theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.”
Alisema kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya
(1) “kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya sheria maana
yake ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na
kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha
matumizi ya masharti hayo”.
“Pingamizi limepelekwa mahakamani kutokana na tume
kushindwa kuzingatia masharti ya Katiba yaliyowekwa na ibara hii, ibara
ya 98. Vilevile tume imeshindwa kuzingatia masharti ya hadidu za rejea
yaliyowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura 83,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Kalokola, katika kutunga sheria
ya kuunda Bunge la Katiba Serikali imelipotosha Bunge kwa kuunda sheria
ambayo haikuzingatia masharti ya uhalali wa uwakilishi kama yalivyowekwa
na Katiba hususan ibara ya 21.
“Kwa mujibu wa uhalali wa uwakilishi, Katiba
inaweka masharti kuwa wawakilishi halali watakuwa ni wale waliochaguliwa
na wananchi kwa hiari yao, kwa haki na uhuru kabisa kwa kuzingatia
utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria,” ameeleza katika
hati hiyo na kuendelea;
“Baya zaidi Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa kwa
mujibu wa sheria uteuzi utalenga kutengeneza Bunge la Katiba lenye sura
ya utaifa kwa kuzingatia mahali wanapoishi wajumbe walioteuliwa. Kwa
uhalisia wajumbe kutoka Tanzania Bara, zaidi ya asilimia 75 wanaishi Dar
es Salaam.”
Dk. Kalokola ameeleza pia kuwa Serikali
iliwapotosha wabunge kutokana na shinikizo la wanaharakati kutunga
sheria ambayo inawapa nafasi wanaharakati kushiriki katika uamuzi wa
Katiba ambayo wananchi wangeipenda.
“Ifahamike kuwa asasi zote za wanaharakati
zimeundwa kwa malengo ya kushinikiza Serikali kukubali matakwa ya
masilahi yao. Baya zaidi wanaharakati wengine ni mawakala wa wakoloni
mamboleo kutoka nchi za nje,” alisema.
Dk. Kalokola alieleza kuwa kesi hiyo imefunguliwa
kupinga posho zilizoahidiwa kwa wajumbe wa Bunge la Katiba, kwa kuwa ni
kubwa mno ikilinganishwa kipato cha taifa.
“Tukumbuke kuwa Serikali imepuuza kuwa ina dhima
kubwa kwa ustawi wa jamii, na wafanyakazi wengine kama walimu
hawajalipwa stahiki zao. Serikali imefanya makosa kutumia fedha kuwa
silaha yetu ya kupata Katiba Mpya. Ifahamike kuwa Baba wa Taifa alisema
kuwa ni fikra potofu kuchagua fedha kuwa silaha yetu, silaha ambayo
hatuna. Mnyonge hawezi kuchagua fedha kuwa silaha yake,” alisema.
Ombi mahakamani
“Tumeiomba Mahakama itoe tamko la kuwalazimisha
wahusika kuzingatia masharti yaliyowekwa na Katiba katika utekelezaji wa
majukumu na wajibu wao na kusimamisha Bunge la Katiba hadi hapo
litakapopatikana Bunge la Katiba lenye uhalali wa uwakilishi
litakolokuwa limechaguliwa na wananachi wenyewe kwa hiari yao kwa haki
na uhuru kabisa,” alisema.

0 maoni:
Chapisha Maoni