Stori: Mayasa Mariwata na Andrew Carlos
MKONGWE wa muziki wa dansi nchini,
Muhidin Mohamed Mwalimu Gurumo ‘Maalim Gurumo’ amezikwa jana kwenye
makaburi ya kijijini kwake, Masaki, Kisarawe mkoani Pwani, lakini wosia
aliouacha kuhusu mazishi yake umezua utata, Risasi Mchanganyiko
limedokezwa na wengi.
Kwa mujibu wa chanzo, wakati wa uhai
wake Maalim Gurumo ambaye alikuwa mwanamuziki wa bendi mbalimbali
nchini, ikiwemo Ottu na baadaye Msondo Music Band, alisema
atakapotangulia mbele ya haki asizikwe siku inayofuata.
LIMWAMBIA NANI?
Kwa mujibu wa chanzo, Gurumo alimpa
wosia huo mjomba’ake aitwaye Selemani Mikole ambaye ndiye aliyemlea
alipofika jijini Dar es Salaam baada ya kufiwa na baba yake mzazi, mzee
Mohamed Mwalimu Gurumo.
“Gurumo alikataa kuzikwa siku inayofuata. Mjomba wake ndiye aliyetoa siri hiyo mara baada ya Gurumo kufariki dunia.
“Yaani alitaka hivi, mfano amefariki
dunia leo (jana Jumanne) basi mazishi yake yawe baada ya siku mbili,
yaani keshokutwa (Alhamisi).
“Mjomba’ake alimuuliza sababu ya uamuzi
huo, akasema yeye ni mtu mwenye mashabiki wengi, angeomba pawe na muda
ili wengi waweze kuhudhuria mazishi yake,” kilisema chanzo hicho.
WAISLAM WATOFAUTIANA
Jumatatu iliyopita kwenye msiba wa nguli
huyo nyumbani kwake, Mabibo-Makuburi jijini Dar es Salaam baadhi ya
waombolezaji wenye imani ya Kiislam walisikika wakipingana na wosia huo
wa marehemu.
Baadhi walisema si sawa Muislam kuzikwa
baada ya saa ishirini na nne huku wengine wakisema wosia wa marehemu
ndiyo maelekezo makuu ya mazishi.
“Hapa hatuzungumzii sheria za dini,
tunazungumzia kutii wosia wa marehemu. Siku zote wosia wa marehemu
unazingatiwa kwanza,” alisikika akisema mwombolezaji mmoja baada ya
kuambiwa mazishi ya marehemu huyo ni Jumanne na si Jumatatu kama
alivyoamini.
UISLAM UNATAKAJE?
Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya
kuzungumza na baadhi ya viongozi wa Kiislam wa jijini Dar es Salaam
ambapo kila mmoja alitoa mwongozo wake anaoujua kuhusu imani ya Kiislam
inavyosema kuhusu mazishi ya muumini wake.
“Kwenye Uislam kuna ngazi tatu tu baada
ya kifo. Kuoshwa, kuswaliwa na kuzikwa. Kama mtu anakata roho asubuhi na
madaktari wakathibitisha, mwili wake hautakiwi kulala,” alisema shehe
mmoja huku akiomba kusitiriwa jina.
MAALIM HASSAN NAYE ALONGA
Risasi Mchanganyiko pia lilizungumza na
mtabiri maarufu nchini kwa sasa, Hassan Hussein Yahya ‘Maalim Hassan’
ambaye kwa upande wake aliweka wazi mambo haya:
“Kusema kweli Uislam mwili haulali.
Labda kama mtu amekutwa na mauti usiku, lakini siku inayofuata lazima
akasitiriwe (akazikwe).
“Endapo kuna dharura sana, basi zisipite
saa ishirini na nne tangu kifo. Lakini hilo la Gurumo sidhani kama ni
tatizo, unajua imani ipo, lakini pia tunaheshimu mila na desturi zetu
Waafrika.”
SHEHE MKUU MKOA WA DAR ES SAALAM
Gazeti hili pia lilizungumza na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum ambapo alisema:
“Katika Uislam hakuna sheria kwamba mtu
akifa lazima azikwa siku hiyohiyo, wala hakuna siku zilizotajwa kuwa
ndizo za marehemu kuwepo kabla ya mazishi. Ila kumzika marehemu mapema
ni suna.
“Mbona Mtume Mohamed (S.A.W) alikufa Jumatatu akazikwa Jumatano?”
KUMBE SI DHAMBI
Pia Risasi Mchanganyiko lilizungumza na
baadhi ya Waislam wanye elimu ya imani hiyo kwa undani ambapo wengi
walisema mwili wa marehemu kuzikwa ndani ya saa 24 ni sheria ya kawaida
lakini si dhambi kama ikitokea ukapitiliza saa hizo.
ALIJITABIRIA KIFO?
Akizungumza na gazeti hili juzi kwa
majonzi makubwa, mtoto wa marehemu aitwaye Mariam Gurumo alisema baba
yake ni kama alijitabiria kifo kwani Aprili 9, mwaka huu (siku nne kabla
ya kifo) walikwenda Kisarawe kwa ajili ya kusalimia ndugu, jamaa na
marafiki na kurudi Dar.
“Hiyo safari ilikuwa niende mimi.
Nikaenda nyumbani kumuaga, lakini akasema lazima twende familia yote.
Basi tukajaza mafuta kwenye lile gari alilozawadiwa na Diamond (Toyota
FunCargo) tukaenda.
“Tulipofika, baba akazua tukio jingine,
akasema lazima tutembelee makaburi ya familia kwa ajili ya kuyasafisha
na kupiga dua kuwaombea marehemu waliolala pale jambo ambalo kwetu sisi
watoto tulilishangaa,” alisema mtoto huyo.
Akaendelea: “Lakini tulipojiandaa kwenda
makaburini, mvua kubwa ilinyesha. Kwa hiyo tukamwacha baba tukaenda
sisi kufanya shughuli hiyo.
TATIZO LAANZA HADI KIFO
Mtoto huyo aliendelea kuweka kwamba,
wakati wanarudi kutokana na milima na mabonde ghafla hali ya mzee Gurumo
ikawa mbaya. Walipofika Msanga akaomba kwenda kujisaidia. Mara mvua
kubwa ikanyesha tena naye akanyeshewa na kulowa chapachapa.
Alisema kuwa, hali hiyo ilimsababishia
mzee Gurumo kuzidi kudhoofu zaidi kutokana na tatizo la mapafu kubana na
kushindwa kupumua sawasawa.
“Tulifika Dar, hali ikazidi kuwa mbaya
ndipo ikatulazimu kumkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya
matibabu ambapo Jumapili akafariki dunia majira ya saa tisa alasiri,”
alisema mtoto huyo.
GPL
Home
»
»Unlabelled
» WOSIA WA GURUMO WAZUA UTATA
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)

0 maoni:
Chapisha Maoni