About

www.facebook.com/archileusanatory/pambazuabongo


Serikali imepanga kununua rada nyingine mbili zitakazogharimu Shilingi bilioni 11.14 katika mwaka wa fedha wa 2014/15.

Hatua hiyo inakuja wakati makovu ya kashfa ya rada ya awali iliyonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu, yakiwa hayajapona.

Nia hiyo ya serikali ilitangazwa juzi na Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe, wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Itakumbukwa kuwa rada hiyo ya mwanzo ilinunuliwa kwa bei ya Dola milioni 40 ( Pauni za Uingereza milioni 28) na iliibua kashfa iliyowezesha chenji ya Shilingi karibu bilioni 30 kurejeshwa nchini na kutumika kuboresha elimu kwa mujibu wa masharti ya Uingereza iliyorudishwa fedha hizo.

Waziri alisema rada hizo ni za kuongoza ndege za kiraia na mazungumzo yanaendelea baina ya serikali na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga(ICAO) ili kupata rada hizo kutoka kwa watengenezaji.

Rada ya jeshi iliyonunuliwa siku za mwanzo ilipatikana kupitia kwa wakala aliyelipwa zaidi ya Shilingi bilioni 12 na kukinunua kifaa hicho kwa gharama ya Dola milioni 40 kutoka kampuni ya Uingereza ya Kutengeneza Vifaa vya Kijeshi ya BAE Systems

Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya kushughulikia makosa makubwa ya rushwa (SFO) ya Uingereza ilibaini kuwapo utapeli huo na kesi ilipofikishwa mahakamani iliamuliwa Tanzania kurudishwa fedha zake.

Wakati huo huo, katika jitihada za kuboresha usafiri jijini Dar es Salaam, Wizara ya Uchukuzi inakusudia kutumia wawekezaji binafsi kusafirisha abiria kwa treni.

Waziri wa Uchukuzi Dk Mwakyembe, alisema wawekezaji hao watahusishwa kupitia ubia baina ya sekta ya umma na ya binafsi (PPP).

Aliliambia Bunge kuwa makampuni mengi kutoka ndani na nje ya nchi yameonyesha nia ya kutoa huduma hiyo na kwamba kwa kushirikiana na Kampuni ya Reli (TRL) Shirika Hodhi la Rasilimali za Reli (Rahco) serikali itaanzisha kampuni tanzu ya ya usafiri wa treni unaowashirikisha wawekezaji binafsi.

Usafiri wa treni jijini Dar es Salaam unaendeshwa na TRL kwa kushirikiana na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kwa kutoa huduma zake kuanzia stesheni za Ubungo Maziwa hadi Stesheni kwa upande wa TRL.

Aidha Tazara nayo hutoa huduma hizo kuanzia Mwakanga hadi Kurasini.

UPANUZI WA HUDUMA ZA TRENI DAR
Akizungumzia kuongeza huduma hizo ili kupunguza foleni alisema kamati maalumu ya wizara hiyo inayoshughulikia usafirishaji huo, imechambua, kuanisha mipango na mikakati ya kuboresha na kupanua huduma ya usafiri wa treni ya abiria jijini na kuweka mikakati ya utekelezaji.

“Mikakati iliyoainishwa ni kuongeza eneo la ujenzi wa miundo mbinu kutoka urefu wa kilometa 20 za sasa hadi kufikia kilometa 50 ili kuzijumuisha wilaya za Kibaha, Kisarawe, Mkuranga, na Bagamoyo” alisema Waziri.

Aliliambia Bunge kuwa wazabuni tisa wamejitokeza kufanya upembuzi yakinifu wa kupanua huduma hiyo ya treni ya abiria kuifikisha Kibaha , Bunju, Mbagala na Pugu na kwamba sita kati ya hao wamewasilisha maandiko ya kina kuhusu utekelezaji mradi huo.

“Uchambuzi wa maandiko yao unaendelea lengo likiwa ni kumpata mtaalamu mwelekezi wa mradi huo ndani ya mwaka mpya wa fedha ” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza kuwa kuna mpango wa kujenga njia mpya ya reli ikiwamo ya kwenda maeneo ya Pugu , Mbagala/Chamazi, Luguruni/Kibaha na Bunju/Kerege na pia ujenzi wa mchepuko wa njia ya reli kutoka kituo cha Ilala hadi Stesheni ili kuepusha mwingialiano wa treni ya abiria ya Stesheni Ubungo Maziwa na ile ya mizigo kutoka Kurasini(bandarini).

CHANZO: NIPASHE

0 maoni:

Chapisha Maoni

 
Top