Watu wawili wa familia moja Frank Charles na mkewe Asia Khamis
wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya shilingi
milioni moja kila mmoja kwa kosa la kukutwa na madawa ya kulevya aina ya
bangi.
Hakimu wa mahakama ya wilaya ya Mbeya Maria Batulaine amewatia
hatiani wanandoa hao baada ya kuridhishwa na ushahidi usio shaka wa
mashahidi wanne wa upande wa mashitaka.
Imedaiwa na Mwendesha mashitaka wa Serikali Juliana William amesema
kuwa washitakiwa hao walikutwa na kete 100 za bangi Novemba 19 mwaka
jana eneo la Makunguru Jijini Mbeya baada ya upekuzi wa Polisi.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili aliwapa washitakiwa nafasi ya
kujitetea ambapo walisema kuwa wana watoto wawili mmoja akiwa darasa la
nne na mwingine akiwa kidato cha tatu hivyo kuiomba mahakama kuwaangalia
kwa jicho la huruma kwa kuwa hilo ni kosa lao la kwanza.
Wakati Hakimu Batulaine akitafakari adhabu kwa washitakiwa hao
mshitakia wa pili Asia Khamis alianguka ghafla kizimbani na kuzirai na
kumwacha Hakimu akiwa kimya kwa muda kabla ya kutoa hukumu.
Mwendesha mashitaka Juliana William aliiomba mahakama kutoa adhabu
kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya
kuvuta na kuuza madawa ya kulevya.
Hakimu Maria Batulaine aliwahukumu kwenda jela miaka mitano jela au
kulipa faini ya shilingi milioni moja kila mmoja na mshitakiwa wa
kwanza alikuwa akihaha kutafuta fedha hizo na baadhi ya wasamaria
walikuwa wakitoa huduma kwa mkewe baada ya kudondoka kizimbani na
kuzirai.


0 maoni:
Chapisha Maoni