PATASHIKA nguo chanika inaendelea kichini chini
kwa vingunge wa vyama vya siasa kuendesha kampeni za urais kwa uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015. Majina kadhaa yanatajwa na wao kutokanusha,
na wapambe wao kuzizima.
Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa
Waziri Mkuu Mstaafu (kwa kashfa), Edward Lowassa, Waziri wa Afrika Mashariki,
Samwel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard
Membe, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na wengineo
wachache.
Kwa vyama vya upinzani, anatajwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa, Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wakati kwa
upande wa Chama cha Wananchi (CUF), anatajwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim
Lipumba. Wote wanaojinasibu na kinyang’anyiro hicho, wanatoka Bara. Wazanzibari
hawatajwi, kana kwamba Zanzibar si sehemu ya Tanzania.
Kwa CCM, ni utamaduni uliozoeleka kwa mgombea
kutokana na Kamati Kuu ya Chama hicho, lakini kinyume na matarajio, hao
wanaotajwa kuukamia urais wamefyekwa katika Kamati hiyo kwa sababu
zisizofahamika.
Kuteuliwa kwenye Kamati Kuu ya CCM kwa mwanasiasa
mkongwe na mwanadiplomasia wa kimataifa, Dk Salim Ahmed Salim bila matarajio ya
makada wengi wa chama hicho, kumezua minong’ono, kiwewe na taharuki kwa
wanyemeleaji wa nafasi hiyo kwamba huenda Dk Salim anaandaliwa kwa mambo
makubwa zaidi. Hata hivyo, wanajiliwaza kwamba kwa umri wake wa miaka 73,
Dk Salim hizi si zama zake za kuongoza nchi!
Lakini pamoja na hayo, wanafahamu kwamba katika
hali ya sasa ya taifa kupoteza dira na mwelekeo, panahitaji Rais makini
kutawala awamu moja tu ili kuweka mambo sawa, bila kujali umri wala itikadi ya
chama chake, mradi tu awe mzalendo na mkombozi wa wanyonge.
Lakini Mungu si Athumani; lolote laweza kutokea
kwa mazingira ya sasa ya kuchafuka kwa bahari ya kisiasa, kiuchumi na kijamii,
hivyo kuhitaji nahodha mkongwe kuinusuru meli kwenye tufani. Tayari CCM imeweka
wazi kuwa kinakusudia kurejea kwenye misingi ya uadilifu wa enzi za TANU na ASP
ili kurejesha heshima ya taifa hili.
Ni nani awezaye kufufua misingi hiyo kwa uhakika
na umakini mkubwa mbali na wa zama za Dk Salim Ahmed Salim? Jukumu hilo muhimu,
kama tunavyoshuhudia, haliwezi kutekelezwa na wanasiasa wa zama za ‘Bongo
fleva,’ au wale wanaotamba kwa ufisadi wao nchini. Taifa linayumba kwa kukosa
viongozi wenye busara na hekima.
Taifa liko njia panda likiweweseka kwa dhambi kuu
nne za maangamizi. Mosi; ni nchi kukosa itikadi na dira ya maendeleo. Tunaimbishwa
Ujamaa huku tukichezeshwa ngoma ya Ubepari, ya kila mtu kuishi kwa ukali wa
meno yake. Pili; ni kutoweka kwa maadili na utamaduni wa taifa hili kwamba nchi
inabugia sumu, makapi ya kila aina kwa maangamizi yake. Nchi inapokosa
utamaduni wake, ni sawa na mti usio na mizizi, kuweza kuangushwa na upepo duni
tu.
Tatu; ni kutoweka kwa heshima ya Mtanzania katika
duru za kimataifa, tofauti na enzi za Serikali ya awamu ya kwanza ambapo
alisifika kama mpigania haki, usawa wa kijamii, amani na utulivu. Nne; ni
kuibuka kwa udini unaotishia kuipasua nchi vipande vipande, na pengine kuitupa
kwenye janga la umwagaji damu.
Tano; ni kero za Muungano ambapo Zanzibar sasa
inataka itambuliwe kama nchi. Tayari Wazanzibari wamezika tofauti na uhasama
wao wa siku nyingi na kufanikiwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa; uhasama
uliowagawa na kuwadhoofisha kisiasa na kijamii kuweza kufinyangwa finyangwa
ndani ya mfumo tata wa Muungano.
Leo wanaweza kuzungumza kwa herufi kubwa ndani na
nje ya Muungano; na tayari wamesema sasa ni zamu yao kutoa Rais wa Muungano.
Je; Wabara ambao ndio walio wengi, watakubali hilo, katikati ya mikanganyiko ya
kisiasa na kidini inayolikumba Taifa letu hili?
Misingi ya TANU na ASP ndiyo iliyozaa kile
tunachojivunia sasa kama ‘hali ya amani na utulivu’ ambavyo vinatoweka haraka
kutokana na uongozi wa nchi kuwa mikononi mwa nyang’au walafi na ubinafsi.
Misingi hiyo ilikuwa ni usawa wa binadamu, vita dhidi ya rushwa, unyonyaji,
uonevu na maisha bora kwa wote.
Chama Tawala kama CCM, hakiwezi kusalimika kama
Chama iwapo wanachama wake, hasa viongozi, watautazama utendaji wake (Dk Salim)
kwa maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya umma. Uanachama na uongozi wa aina
hiyo, ni ugonjwa (ukoma) ndani ya Chama.
Kinachopotea haraka hivi sasa, kwanza; ni uhuru
wa kitaifa, kwa maana ya uwezo wa wananchi kuamua juu ya hatima yao ya
kujitawala bila kuingiliwa na watu wasio wazalendo. Pili; ni kupotea kwa uhuru
dhidi ya njaa, magonjwa na umasikini kwa kuwa tu siasa, uchumi wa nchi na
rasilimali za Taifa zimehodhiwa na kikundi kidogo cha wahujumu uchumi na
mafisadi na Serikali ikasalimu amri kwa wadhalimu hao.
Tatu; ni kutoweka kwa uhuru binafsi, haki ya
kuishi maisha ya heshima na usawa kwa wote, uhuru wa mawazo na wa kushiriki
katika maamuzi yanayogusa maisha ya watu. Hivi leo, mambo hayo ni kwa
kudra ya Mungu, kwa kuwa kundi la walionacho halimjui mdunda kazi mwenye njaa.
Na ingawa kuna Bunge linalopashwa kumsemea, limetekwa na ufisadi na
kujipambanua kama taasisi ya ulaji na ya kuzika demokrasia.
Kurejea kwa wakongwe wenye kumbukumbu sahihi ya
mambo haya kwenye ulingo wa CCM, kama vile Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa,
Philip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mohamed Seif Khatib na
wengineo, ambao hapo nyuma walipigwa buti kuachia nafasi vijana (ma-bongo
fleva), ni ishara ya kutambua usemi kwamba ‘lazima utazame nyuma ili uweze
kwenda mbele,’ na ni dalili pia ya kushindwa kwa kizazi kipya kuongoza nchi kwa
mafanikio bila kuingiza busara na hekima ya wakongwe.
Ilivyo sasa, CCM imegeuka kokoro lenye kuzoa kila
uchafu na kutishia amani na usalama wa taifa kutokana na ukweli kwamba Chama
lege lege huzaa Serikali legelege!
Kwanini tusiwe na kina Salim Ahmed Salim na kina
Philip Mangula, Mohamed Seif Khatibu na wengineo wachache, kurejesha heshima ya
Taifa hili baada ya kizazi cha ‘Bongo fleva’ kuonyesha wazi kushindwa kuhimili
changamoto za utawala wa nchi?
Kuongoza nchi bila itikadi wala maadili ya taifa,
ni sawa na nahodha asiyejua bandari aendayo. Kwa nahodha kama huyo, hakuna
upepo ulio mwafaka kwake. Na ndimo tulimo hivi sasa, kwa nchi yetu kugeuzwa
shamba la bibi pasipo mtu wa kukemea; uzalendo unayoyoma haraka kwamba
tusishangae kuona siku moja Bunge likiongozwa na Spika Mjapani, au nchi kuwa na
Waziri Mkuu Mmalaysia, kadri tunavyozidi kuruhusu nguvu ya fedha kuchukua
nafasi ya uzalendo, kwani tayari wahaini hawa wanazungumzia uraia popo wa nchi
mbili!
Nchi inakabiliwa na janga hatari jipya la
mgawanyiko kwa misingi ya udini na uhasama unaokithiri, kati ya Wakristo na
Waislamna kutishia amani. Haya yote ni ishara ya kudhoofika kwa uzalendo, umoja
wa kitaifa na kiitikadi.
Kama hali hii itaachwa kuendelea, uchaguzi mkuu
ujao utakuwa mgumu kwa sababu kila kundi litataka achaguliwe Rais wa dini yake
kwa gharama ya utaifa. Kwa hali ilivyo, hakuna mgombea mwingine anayeweza
kuleta suluhu ya makundi haya mawili zaidi ya Dk Salim Ahmed Salim ambaye
anakubalika kwa Wakristo na kwa Waislamu; tangu kale, juzi, jana hadi leo.
Dk Salim si mdini, si mhafidhina wa kisiasa, ni
mwanademokrasia jamii. Kikundi cha Wazanzibari, kilichojiita ‘Liberators’
(Wakombozi) na kuzoea kumhujumu ili kulinda ‘ukale’ kinajua hilo na hakimuwezi
tena.
Na kwa kuwa Wazanzibari sasa wamezika tofauti zao
za kiitikadi za miongo mingi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sasa ni
dhahiri zile hujuma walizokuwa wakimfanyia Dk Salim, kwamba yeye ni mwanachama
wa zamani wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) hazina mshiko tena.
Kwa sababu hiyo, anaweza kuwa mgombea pekee wa
urais, akipenda, anayekubalika vizuri na pande zote za Muungano pamoja na
makundi ya kidini yanayoibuka kuliko mwanasiasa mwingine yeyote yule, Bara na
Visiwani, licha ya umri wake mkubwa.
Heshima ya Mtanzania imeporomoka mara dufu
kimataifa tangu enzi za awamu ya pili. Kiongozi wa Kitanzania wa sasa si yule
wa enzi za awamu ya kwanza, aliyechukia udhalimu, uonevu, unyanyasaji na
ukoloni wa kimataifa, bali viongozi wa sasa ni mazuzu tegemezi, wasaliti na
wakumbatia rushwa, ufisadi na mamluki wanaonunulika kirahisi kwa maangamizi ya
nchi na wananchi.
Kuna mantiki gani kupinga maoni yaliyotolewa na
Mwingereza, Bi Sarah Hermitage hivi karibuni kuhusu ufisadi, dhuluma na rushwa
serikalini? Kuna mantiki gani kwa mafisadi wa nchi hii kuchochea vijana
waandamane dhidi yake kwa madai ya kutudhalilisha badala ya kumsapoti?
Watuambie, iko wapi chenji ya vijisenti vya rada
tuliyoambiwa vitalipwa? Kwa nini tunaficha nyuso juu ya ufisadi mkubwa wa
Meremeta, Richmond/Dowans, Deep Green na mwingine wa aina hiyo? Wanafiki wapevu
hawa! Wahaini, wasaliti wa taifa!
Tumejenga utamaduni tata wa kupata marais
kutokana na mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje, kuanzia na Rais Mstaafu Benjamin
Mkapa, Rais wa sasa Jakaya Kikwete; na leo Waziri wa sasa wa wizara hiyo,
Bernard Membe anapiga jaramba kufuata nyayo.
Yote haya eti ni kwa lengo la kutia ubani uvundo
wa nchi katika medani za kimataifa! Kama kweli hiyo sasa ndiyo tiketi ya urais,
basi hakuna Mtanzania aliye hai wa kuweza kumfikia Mwanadiplomasia Dk Salim
Ahmed Salim!
Dk Salim Ahmed Salim, kama alivyokuwa Mwalimu
Julius Nyerere, ni mwanasiasa, mwanadiplomasia wa kimataifa na msomi mwenye
historia ndefu ya harakati za mapambano dhidi ya uonevu; mwenye kiu ya haki na
usawa kwa wote. Wengi tunamkumbuka miaka ya karibuni kama Balozi, Waziri Mkuu
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (sasa Umoja wa Afrika) na
msuluhishi wa migogoro kimataifa.
Mwamko wake wa kisiasa unaanzia miaka ya 1950
huko Zanzibar enzi za mapambano ya kudai uhuru wa visiwa hivyo, kama Katibu
Mwenezi wa Umoja wa Vijana uliojulikana kama Youths Own Union (YOU), uliounga
mkono harakati za chama cha mrengo wa kushoto cha Zanzibar Nationalist Party
(ZNP).
Wakati huo, vijana wa Kizanzibari walijipambanua
na harakati za kupinga ukoloni kitaifa na kimataifa, kuanzia harakati nchini
Algeria dhidi ya ukoloni wa Kifaransa, na Ghana dhidi ya Waingereza, Mau Mau
(Kenya) na Afrika kusini dhidi ya tawala za kibaguzi za Wazungu, na kutoka
harakati za ukombozi wa Wapalestina hadi vita ya Vietnam, kwanza dhidi ya
Wafaransa na baadaye Marekani.
Dk Salim, kama msemaji wa YOU, alikuwa mtu wa
kwanza Afrika Mashariki kutahadharisha juu ya uwezekano wa Waziri Mkuu wa
Kwanza wa Congo, Patrice Emery Lumumba, kuuawa na mabeberu, ilipotangazwa
kwamba amepotea. Alishambulia (Dk Salim) vikali Shirika la Ujasusi la Marekani
(CIA) kwa hujuma hiyo; na leo historia imethibitisha kuwa alikuwa sahihi.
Ni Dk Salim aliyewaongoza vijana wa Kizanzibari
kupinga hatua ya Marekani kujenga Kituo cha Kijasusi (tracking station)
Zanzibar sehemu ya Tunguu, hadi kikaondolewa. Ni katika harakati hizi dhidi ya
ukoloni na ubeberu, alikutana na mwandani wake, Mama Amne Ali Rifai wakaoana.
Ni kutokana na kuundwa kwa chama cha harakati za
ukombozi cha Umma Party visiwani Zanzibar, kwa vijana wanaharakati kujiengua
kutoka ZNP, wakiongozwa na Abdulrahman Babu mwaka 1963, kwamba Dk Salim alianza
mikiki mikiki ya kibalozi, kwanza nchini Cuba na baadaye Misri.
Alikuwa Cuba wakati Rais wa nchi hiyo, Fidel
Castro alipotangaza azimio lake mashuhuri la Havana (the Havana Declaration),
na Dk Salim akalikariri sehemu zake muhimu kwa lugha ya Kihispaniola. Baada ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, Serikali mpya ya Mapinduzi ilimteua
kuwa Balozi nchini Misri akiwa na umri wa miaka 22 tu. Na Muungano waTanganyika
na Zanzibar ulipozaliwa, Aprili 1964 alibakia Misri kama Balozi wa Tanzania.
Alitumika kama Balozi kwa mara ya mwisho nchini
China ambako alikuwa rafiki kipenzi cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo,
Chou-en-Lai, kabla ya kuteuliwa Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa (UN), alikotumikia kwa miaka kumi.
Akiwa huko, alitoa mchango mkubwa na kuiletea
heshima kubwa nchi yetu, kwanza kwa kuchaguliwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya
UN ya Ukombozi dhidi ya Ukoloni, kisha Rais wa Baraza la Usalama la UN na Rais
pia wa Baraza Kuu la Umoja huo.
Aliwania nafasi ya Katibu Mkuu waUN na kuungwa
mkono na mataifa yote wanachama, lakini alishindwa kwa kura turufu (Veto) ya
Marekani kwa sababu tu alijipambanua na siasa za mrengo wa Kisoshalisti. Ndiyo
kusema kwamba mchango wa Dk Salim kwa ukombozi wa Bara la Afrika na dunia kwa ujumla,
hauwezi kupuuzwa wala kusahaulika.
Kama Watanzania wanatafuta Rais wa kurejesha
amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa, usawa na demokrasia ya kweli nchini na
heshima inayopotea, ni nani zaidi ya Mtanzania huyu asiyejua lugha ya ulafi,
ufisadi, udini wala kulipiza kisasi, Dk Salim Ahmed Salim? Tunahitaji mtu wa
aina yake kwa kipindi kimoja tu cha uongozi kunusuru nchi yetu!
Joseph Mihangwa

0 maoni:
Chapisha Maoni