Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza,
akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Msajili Mkuu, Jaji
Francis Mutungi, alisema kuwa ofisi yake inafuatilia tuhuma za kutekwa
kwa paroko huyo maarufu kama Father Kizito, ambaye anawahusisha
wanachama wa CCM, akidai pia walimwekea pilipili na sindano ya kushonea
viatu mfukoni.
Aidha, ofisi hiyo imesema wanamsaka
mgombea ubunge wa Chama cha Chausta, Richard Minja, ambaye alichukua
fomu kuwania nafasi hiyo, lakini ameshindwa kutokea hadharani na kuwapa
ushirikiano ikiwamo kuhojiwa na kuendelea na mikutano ya kampeni ambayo
itasitishwa Machi 15.
“Tumewahoji wagombea wa vyama vyote
viwili vya CCM na Chadema kuhusu mwenendo mzima wa kampeni zinazoendelea
katika jimbo la Kalenga ili kupata maoni yao na taarifa nyingine kuhusu
matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa sheria…Hili la
Paroko kutekwa na kujeruhiwa tunalifuatilia kujua ukweli na tutachukua
hatua stahiki ili kutoa uwanja sawa wa haki kwa kila upande,” alisema
Nyahoza.
Father Kizito, anadaiwa kukamatwa na
kutekwa na watu hao kabla ya kujeruhiwa juzi, majira ya saa 11 jioni kwa
madai ya kukisaidia Chadema.
Ofisi hiyo imesema itakutana na wadau
wake ili kueleza nia yake ya kuvilazimisha vyama vyote vyenye vikosi
vya ulinzi vya vyama kuvivunja mara moja kabla ya kuelekea katika
uchaguzi mkuu mwakani kwa kuwa chanzo cha machafuko au uvunjifu wa amani
katika chaguzi hizo ni vikosi hivyo.
“Tunavitaka vyama vya siasa vyenye
usajili wa kudumu na visivyo na usajili wa kudumu, havitakiwi kuendelea
kuwa na vikosi vya ulinzi kwa madai ya kujilinda wenyewe kutokana na
Jeshi la Polisi kudaiwa kushindwa kutoa ulinzi wanaoutaka na badala yake
vinaamua kujilinda vyenyewe.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alipoulizwa na NIPASHE
kuhusiana na tuhuma hizo kuwasilishwa kwa Msajili wa vyama vya siasa,
alidai kwamba tukio hilo ni la kupangwa na limetengenezwa na Chadema.
“Wanataka kupotosha maana wakati
kiongozi huyo wa dini anakamatwa CCM hawakuwepo eneo hilo na
waliomkamata si viongozi na wala si makada wetu na kwa maana hiyo tukio
lenyewe ni la kupangwa na Chadema.
Wanatengeneza kwa sababu huyo bwana
(Father Kizito) alikuwa na gari la M4C…Na itapendeza sana kama
utawauliza pia na wananchi wenyewe ni nini kilichotokea. Hayo ni mambo
ya kiuzushi,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Ramadhan Mungi, aliiambia NIPASHE kuwa Polisi imeanza
uchunguzi wa tukio hilo na iwapo tutabaini kuna chama kimehusika katika
tukio hilo kwa lengo la kujinufaisha kisiasa kwa wapiga kura tutachukua
hatua za kisheria dhidi ya wahusika,” alisema.
Chanzo:- NIPASHE


0 maoni:
Chapisha Maoni