Wakati tukio la kupotea kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Malaysia, MH370, linaendelea kuitikisa dunia,
imebainika kuwa Tanzania si jambo jipya kutokana na kuwapo kwa
kumbukumbu ya matukio manne tofauti kama hayo katika miongo minane
iliyopita.
Ndege hiyo ya Malaysia ilipotea wiki
mbili zilizopita ikiwa na abiria 227 na wafanyakazi 12 huku juhudi za
kuitafuta zinazofanywa na nchi 26 zenye uwezo mkubwa wa kiuchunguzi
zikiwa hazijazaa matunda.
Kwa matukio ya Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa
Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura amesema
katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu kuwa Tanzania imewahi kuingia
katika kumbukumbu za ndege ndogo kupotea na baadhi hazikuonekana
kabisa na nyingine zilionekana baada ya miaka kadhaa kupita. Ndege ya
kwanza kupotea ilikuwa mwaka 1937 iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda
Madagascar. Ilikuwa na abiria wanane na haijaonekana hadi leo.
Mbali na tukio hilo ambalo limedumu kwa
miaka 77 sasa, Nyamwihura alisema tukio la pili ni la mwaka 2003 wakati
ndege iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Zambia ilipopotea ikiwa na raia
wawili wa Afrika Kusini, nayo pia haijaonekana hadi sasa.
Mkaguzi huyo alisema katika matukio
mengine mawili, ndege zilizopotea zilionekana baadaye. Mwaka 1997, ndege
ndogo iliyokuwa na abiria mmoja ilipotea katika bonde kwenye kilele cha
Kibo, Mlima Kilimanjaro baada ya kutumbukia kwenye korongo na kuganda
kwenye barafu bila kuonekana hadi baada ya miaka sita. Hata ilipoonekana
haikuwezekana kutolewa.
“Ndege ile ilikuwa ikitoka Nairobi kwenda Zanzibar ikiwa na rubani wa Kitanzania peke yake,” alisema Nyamwihura.
Ndege nyingine iliyoingia katika orodha
hiyo ni ile iliyoanguka katika Ziwa Victoria mwaka 1976 ikiwa na abiria
12 ambayo ilionekana miaka miwili baadaye.
Kwa nini ndege zinapotea?
Swali hili linajibiwa na Nyamwihura
akisema sababu kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na
kuharibika kwa miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa
mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.
“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege
hugonga milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu
kupatikana kwa sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama
kwenye makorongo,” alisema.
Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya
ndege ambazo hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi
kwa sababu ama za kigaidi au magendo.
Alitoa mfano wa tukio la mwaka 1945,
wakati ndege iliyokuwa ikitoka Malawi kwenda Nairobi, ilipopoteza
mawasiliano ikiwa katika anga la Tanzania. Baadaye ilibainika kuwa
rubani alifanya hivyo kwa makusudi ili ashushe bidhaa za magendo
alizokuwa amepakia.
Sheria za anga za Tanzania zinakataza
rubani kukata mawasiliano kwa makusudi na adhabu yake ni kufungiwa
kabisa shughuli za urubani.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Moses Malaki alisema
kwa kawaida ndege zinapokuwa angani hufuata ‘barabara’ ambazo zipo kama
miduara inayoonyesha mpaka wa eneo moja kuingia jingine. “Katika hali ya
kawaida, rubani huwasiliana kwa njia ya nukushi (fax) ili vituo vya
eneo husika ambalo ndege hupita vipate taarifa,” alisema Malaki.
“Endapo rubani atashindwa kuunganisha
mawasiliano kutoka eneo moja na jingine na ikitokea kuna miundombinu
mibovu katika eneo hilo, basi ndege inaweza isionekane na kupotea,”
alisema.
Malaki alisema asilimia 95 ya ndege
huanguka au kupotea kwa sababu ya makosa ya kibinadamu na wala si makosa
ya kimitambo akisisitiza kuwa ndege ndiyo usafiri ulio salama zaidi
duniani.
Chanzo ajali za ndege
Rubani Mtanzania anayeishi Marekani,
Brian Meena alisema katika mahojiano kuwa chanzo cha ajali nyingi za
ndege nchini ni makosa ya kibinadamu na wala si mitambo.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wengi wanaopata ajali hizo ni marubani wazoefu na wala si wanafunzi.
“Kwa mfano, unapokuwa na saa nyingi za
kuendesha ndege lazima uchoke, watu wengi wanaoangusha ndege ni wale
wanaotumia muda mrefu hewani,” alisema. Meena alitaja sababu nyingine
kuwa ni miundombinu chakavu ya viwanja vya ndege na mara chache ndege
zenyewe.
“Inawezekana kabisa kuwa mamlaka ya
ndege inafanya kazi kwa mazoea au kienyeji. Wanatumia njia za kizamani
za usimamizi wa usafiri huu na hawaendi na wakati kwa kununua vifaa vya
kisasa,” alisema.
Alisema usafiri wa ndege ni salama kwa asilimia 99 kutokana na mafunzo ya kina marubani wanayopewa.
“Ndege ni kama mtoto, unamlea, unampa anachotaka na ukifanya hivyo ajali labda itokee kwa miujiza,” alisema.
Home
»
»Unlabelled
» UNAAMBIWA KUPOTEA KWA NDEGE TANZANIA SI JAMBO GENI ..ZILISHAWAHI KUPOTEA NDEGE NNE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)


0 maoni:
Chapisha Maoni