Watu watatu wamepora kiasi kikubwa cha
fedha katika Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni, Dar es Salaam katika
tukio linaloweza kufananishwa na sinema.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio
hilo lililotokea jana saa tatu asubuhi, watu hao wakiwa kwenye pikipiki
moja walifika katika benki hiyo na kuiegesha nje ya uzio, kisha wawili
kati yao wakiwa na silaha waliingia ndani.
Muda mfupi baadaye, walitoka nje wakiwa
na mfuko mkubwa wenye fedha na lakini walipokuwa wakitaka kukimbia,
mfuko huo ulianguka. Hata hivyo, waliuokota na kutokomea kusikojulikana.
Mmoja wa mashuhuda, Ali Lunde alisema:
“Walitoka bila wasiwasi tena hawakupiga risasi wala kumtisha mtu yeyote.
Walikuwa na mfuko mkubwa wa ‘kisalfeti’. Walipopanda pikipiki jamaa
aliyebeba mfuko aliukumbatia kama amepakata mtoto.”
Lunde alisema wakati watu hao wakiondoka
na pikipiki, baadhi ya wafanyakazi wa benki walitoka nje huku wakipiga
kelele kuwa wamevamiwa na majambazi.
“Walitoka nje wakipiga kelele, ndipo
kila mtu akajua walikuwa ni majambazi, kama watu wangekuwa na silaha
wangeweza kuwadhibiti maana wote tuliokuwa hapa tumewaona
wanavyoondoka,” alisema.
Dereva teksi anayeegesha gari lake
karibu na benki hiyo, Herode Munyi alisema aliwashuhudia majambazi hao
wakiingia kwenye benki wakiwa na silaha mkononi, jambo lililomfanya
kuwapa taarifa watu wengine huku akitafuta namba za polisi.
“Baadaye nilifanikiwa kuwaona polisi
hawa wanaotembea na pikipiki nikawaambia lakini kama vile walipitiliza,
hawakwenda moja kwa moja benki,” alisema Munyi.
Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo
walionekana kushangazwa na mazingira ya wizi huo, kwani walisema mlinzi
wa benki hiyo hakuwa na bunduki wala kirungu chochote wakati majambazi
walipovamia.
Mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka
kutaja jina lake, alisema wakati majambazi wanavamia benki hiyo,
hakukuwa na watu wengi waliokuwamo ndani, jambo lililowapa urahisi wa
kutekeleza dhamira yao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alisema tawi hilo la benki
halina polisi wanaolinda baada ya benki hiyo kuwaondoa hofu kwa madai
kuwa halina biashara kubwa.
“Mwaka 2012/2013 waliondoa polisi katika
benki ambazo hazina biashara kubwa ikiwamo hii, lakini kuna haja ya
kurudisha ulinzi wa askari polisi,” alisema Wambura
Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Barclays,
Neema Singo alikana madai hayo akisema benki yake ina mkataba na jeshi
hilo pamoja na ile ya Ultimate Security na kusema wameshangaa kwamba
polisi hawakuwapo wakati tukio hilo lilipotokea.
“Tuna mkataba na polisi wa kulinda
matawi yote. Tunachunguza nini kimetokea,” alisema Singo na kuongeza
kwamba kutokana na tukio hilo, tawi hili litafungwa wakati uchunguzi wa
polisi ukiendelea.
Kamanda Wambura alisema kiwango cha
fedha kilichoibwa bado hakijafahamika na kwamba hesabu zilikuwa
zikiendelea kufanywa, huku juhudi za kuwatafuta wezi hao zikiendea.
“Hakuna aliyejeruhiwa ingawa mfanyakazi mmoja amepelekwa hospitali kutokana na mshtuko,” alisema Wambura.
Mwandishi aliwashuhudia baadhi ya
wafanyakazi wa benki hiyo wakiwa wamelala kwenye gari la wagonjwa
wakipatiwa msaada baada ya kupata mshtuko. Pia polisi walionekana
wakizunguka eneo hilo huku wakiwahoji baadhi ya wafanyakazi
Home
»
»Unlabelled
» UPDATES:MAJAMBAZI WAIBA BENKI YA BARCLAYS MCHANA KWEUPE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)


0 maoni:
Chapisha Maoni