Moja kati ya matukio makubwa yaliyoteka
‘attention’ ya watu wengi ni picha na video zilizowekwa kwenye ukurasa
wa Facebook na boss wa Mtanashati Entertainment, Ostaz Juma zikimuonesha
mwimbaji toka Mwanza PNC akiwa amepiga magoti na kuonesha ishara ya
mikono kama anaomba mbele ya boss huyo aliyetulia kwenye kochi akiwa
amekunja 4.
Picha na video hizo ziliwekwa na Ostaz
Juma mwenyewe kwenye ukurasa wake wa Facebook na kuandika, ““hahaha
jamani mziki ni kazi pnc arudi kuomba msamaha ili aendelee kufanya kazi
mtanashati.”
Haikuchukua muda, watu mbalimbali ambao
ni wadau wa muziki wa kizazi kipya walipaza sauti wakilaani kitendo
hicho kupitia mitandao ya kijamii wakiwemo wasanii mbalimbali ambao
hawakusita kumchana Ostaz kwa kile kilichoonekana kuwa ni kumdhalilisha
mwimbaji huyo.
Lakini wapo mashabiki ambao
waliporomosha matusi kufuatia tukio hilo na habari hiyo kusambaa kwa
nguvu kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyompelekea Ostaz kudai kuwa
siye aliyeziweka picha hizo. Lakini kilichowashitua wengi baadae, ni
pale ilipoonekana post nyingine kwenye ukurasa wake akiwaponda
watangazaji wa Tanzania na wasanii kuwa wanasumbuliwa na njaa.
“Naona watu mmeguswa sana na mimi
kuanika picha ya PNC katika mitandao et, tatizo wasanii wa Tanzania
mnanjaa sana kuanzia watangazaji Radio na wasanii njaa ndizo zinazo
wasumbua...”
Lakini baadae aliongea na Moko Biashara
aka One B wa Times Fm kueleza kuwa ukurasa wake metekwa na wezi wa
akaunti za watu mtandaoni (hackers) na kwamba hiyo sio post yake.
“Daah, nshachanganyikiwa rafiki yangu
watu wamehack akaunti yangu wanaandika matusi wanatukana watu..hadi hapa
mimi nimeshachanganyikiwa hadi hata kuongea siwezi bro.” Alisema Ostaz.
Nadhubutu kusema kwa msisitizo kuwa
picha hizo ziliwekwa na Ostaz Juma kwa jinsi nilivyozifanyia utafiti na
kuzingatia kauli yake aloyoniambia kwa mara ya kwanza, “Ndio PNC
kunipigia magoti na kuniomba radhi, lakini sasa mimi nikaamua kuwaonesha
watanzania kwamba PNC amerudi kweli kuniomba msamaha. Je, kama kweli
PNC alikuwa analalamika ‘Ostaz anafanya kazi zake hanijali hanisaidii…”
Hata hivyo sina uhakika…huenda kweli
hakuandika kauli ya kuwaponda watangazaji na wasanii…nasema huenda kwa
kuwa muda mchache baada ya kudai kuwa akaunti yake ilikuwa imetekwa na
hackers na kubadili ‘password’, aliingia tena na kuifuta post hiyo na
kuandika nyingine ya kuomba radhi na kueleza kuwa ilikuwa imetekwa kwa
kipindi kile. Kwa upande wangu ‘no comment’ kwenye hilo.
Anyways, kwa maelezo yote hapo juu bila shaka umepata picha nzima ya tukio hilo japo kwa ufupi.
Sasa niende moja kwa moja kwenye mada na
lengo langu, mkasa huu unapaswa kuwa zaidi ya somo la kawada kwa Ostaz
Juma na wengine hasa watu maarufu ambao huichukulia mitandao ya kijamii
kama Facebook, Twitter, Instagram n.k kama sehemu fulani tu ya kuandika
unachotaka kama jinsi ulivyopewa uhuru ‘What’s on your mind’. Kumbe
unatakiwa kufikiria sana kabla hujaandika na sio kuandika tu kile
kilichoko kichwani kwako, kama unajali.
Ntatumia fikra ambazo nadhani alikuwa nazo Ostaz Juma kabla hajayaona matokeo ya alichokifanyana, matokeo yaliyomchanganya.
Huenda Ostaz Juma alikuwa bado
anafikiria kuwa Radio, Television na magazeti pekee ndio vyombo vya
habari vikubwa kuliko ‘social media’, wazo ambalo ni la kizamani kwa
dunia ya sasa hivi.
Huenda Ostaz alikuwa hafahamu kuwa hivi
sasa kwa kiasi kikubwa Traditional Media kama Radio, Television na
magazeti zimeungana na ‘New Media’ ambazo ni mitandao ya kijamii, tovuti
pamoja na blogs na habari husambaa kwa nguvu kupitia vyombo hivyo huku
vikibadilishana.
Habari nyingi zina-break kwenye mitandao bila kujali muda na huzua mijadala mikubwa kama hiyo.
Huenda alikuwa hafahamu kama,
unachoandika Facebook kikishachukuliwa na watu wakaanza kushare hata
ukifuta bado kitaendelea na kufika mbali zaidi na hata watu kuhamishia
kwenye magroup ambayo huwa na maelfu ya watu au hata kuhamishiwa
‘watsapp’ na huenda wakati unajitetea watu hao wasisikie ama
wakakupuuzia.
Huenda yeye aliona ana marafiki 2,258
akaona sio watu wengi na kwamba isingekuwa issue serious kiivo kama
ambavyo angesema kwenye radio na vituo vya television.
Huenda alikuwa hafahamu kama picha
inaongea lugha zote duniani (universal language) hata bila kufuatilia
nani kaandika nini. Hata mchina atakuwa ameielewa picha hiyo kwa lugha
yake!
Ngoja nimfungue macho kama kweli alikuwa anafikra hizo.
Hadi kufikia mwishoni mwaka jana,
takwimu zilionesha kuwa watu zaidi ya billioni 1.2 duniani kote
wanatumia Facebook na kwamba hao ni active members, na kwa wastani kila
mtumiaji ana marafiki zaidi ya 130 ambao anaweza ku-share nao habari na
ikasambaa duniani kote kwa muda mfupi.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa takribani
asilimia 60 ya watu wazima wanaingia kwenye mitandao mbalimbali ambapo
hata kama hawajajiunga na mitandao ya kijamii wanatembelea tovuti
mbalimbali ambazo zinachukua habari kwenye mitandao ya kijamii.
Habari kama hizo zinazotokea Facebook
huendelea kusambaa pia kwenye mitandao mingine ya kijamii kama
Instagram, na hata Twitter ambayo inachukua 18% ya watumiaji wote wa
mitandao, ambao wengi wao ni ‘active users’ na ndio kundi kubwa la watu
wenye ushawishi (influential) kama watu maarufu. Twitter ina watumiaji
zaidi ya milioni 640.
Kwa upande wa Instagram, kwa mfano
Diamond akiishare picha hiyo wataiona watu zaidi ya 90,000 ambao
wanaweza pia kushare, na huenda watu wakaiamini moja kwa moja habari
hiyo kuwa kuwa msanii wanaempenda kalaani kitendo hicho.
Kwa takwimu hizo, ni vyema kufahamu kuwa
kupitia mitandao ya kijamii hususani watu ambao wanafanya biashara
inayotokana na kuuza kazi zilizobebwa na ‘image’ yao kama vile kazi za
muziki, wanaweza kutengeneza biashara kubwa kwa kuwa wateja wengi
wanaoweza kufanya maamuzi wako kule.
Uamuzi wa kuandika kitu kwenye mitandao
ya kijamii kwa watu wenye biashara kama hiyo nikitolea mfano wa Ostaz
Juma lazima uwe unamnyima uhuru wa kuandika kila anachofikiria tu, bali
kuwaza mara mbili ama tatu matokeo ya kuweka mtandaoni kile
anachofikiria.
Mtu kama Ostaz ambaye anawasaidia
wasanii wa Tanzania, anatakiwa kufahamu kuwa msaada wake kwa wanamuziki
hao kwao ni biashara ambayo inahitaji zaidi ya pesa kwa kuwa wanauza
vitu viwili ambavyo ni muziki na ‘image’. Uropokaji wa mambo unaweza
kuvunja image ambayo kuijenga itamgharimu msanii huyo zaidi ya pesa
alizopewa kurekodi wimbo, kushuti video, kupigishwa pamba na hata pesa
ya promotion.
Kwa mtu maarufu anayetegemea kuuza
kutokana na sapoti ya watu, anatakiwa kufahamu kuwa ukurasa wake wa
Facebook sio kijiwe cha washikaji zake ambacho anaweza kusema chochote
kilicho kichwani kwake bila kujali na wakakipotezea baadae.
Ingawa Radio, Television na magazeti
inawafikia watu wengi zaidi duniani na ina nguvu, ni vyema kwa mtu kama
Ostaz na wengine wenye nafasi katika jamii kuelewa kuwa kila chombo cha
habari kina nguvu kubwa na sio vyema kukilinganisha na chombo kingine
ama kukipuuza.
Yale yalitokea sebuleni kwake (Ostaz Juma) yalipaswa kuwa faragha kwao wote wawili na sio kuyaweka kwenye mitandao ya kijamii.
Mwisho, ni vyema kwa mtu yeyote kutumia
kanuni ya mitandao ya kijamii kuwa usiandike kitu chochote kwenye
mtandao wa kijamii ukiwa na hasira ama ukiwa ‘too emotional’. Jitahidi
kuvumilia kukaa nacho moyoni kwa muda na baada ya kutafakari unaweza
kushare na watu.
Imeandikwa na Josefly Muhozi
Home
»
»Unlabelled
» NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII-CASE STUDY ISSUE YA PNC NA OSTAZ JUMA
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)


0 maoni:
Chapisha Maoni