Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Rais Jakaya Kikwete
amefanya makosa kuhutubia Bunge “kama mkutano wa CCM” na kuipinga
hadharani Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba.
Kikwete alihutubia Bunge la Katiba Ijumaa
iliyopita wakati wa uzinduzi wa chombo hicho maalumu cha kupitisha
katiba mpya, lakini hotuba yake imechukuliwa na wapinzani kuwa ililenga
kutetea maslahi na msimamo wa chama tawala.
Akizungumzia hotuba hiyo, Mbowe alisema Rais alikosea kwa kuwa yeye ndiye aliyeiunda tume hiyo, hivyo kuikosoa siyo sahihi.
Mbowe, ambaye pia ni mjumbe wa Bunge la Katiba,
alisema hotuba ya Rais Kikwete ilikuwa ni sawa na kufungua mkutano wa
CCM, kwani badala ya kuweka mbele masilahi ya taifa aliweka masilahi ya
chama hicho tawala. “Rais Kikwete ametuondoa katika kutetea na kulinda
masilahi ya umma katika Katiba Mpya na sasa ametetea msimamo wa chama
chake,” alisema Mbowe.
Alisema badala ya kujenga maridhiano baina ya
wajumbe, hotuba ya Rais imewagawa zaidi katika misimamo ya vyama vyao.
“Hatujui nini kitatokea baadaye na hatma ya Katiba.. sisi bado
tunajadiliana kama umoja wetu wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) na
tutatoa tamko la pamoja, lakini kikubwa tumesikitishwa sana na hotuba ya
Rais,” alisema Mbowe.
Mbowe alifafanua kuwa Rais Kikwete alikuwa na
nafasi kubwa ya kuwaunganisha wajumbe wa Bunge hilo, kama angehutubia
kama Rais wa nchi badala ya kugeuza Bunge kuwa mkutano wa CCM.
Rais Kikwete alikosoa Rasimu ya Katiba juu ya mapendekezo ya Serikali tatu na ukomo wa ubunge.
Chanzo: Nwananchi
Chanzo: Nwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni