Afafanua utata ulioibuliwa katika taarifa yake mbele ya Bunge la Katiba.
Dar es Salaam. Wakati Ikulu
ikitangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete amevunja Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, tume hiyo imetoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo ya Rasimu ya
Katiba.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilieleza kuwa
Tume ya Jaji Joseph Warioba ilivunjwa tangu Machi 19, ikiwa ni siku moja
baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma.
Wakati taarifa ya Tume ya Warioba ilitolewa jana
jioni, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilikuwa imeshatoa taarifa
ya kuvunja tume hiyo mapema jana ikieleza kuwa shughuli za tume hiyo
zilikoma tangu Jumatano iliyopita.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano alivunja rasmi Tume ya
Mabadiliko ya Katiba tarehe 19 Machi, 2014 kwa Tangazo la Serikali
Na.81 la tarehe 21 Machi, 2014,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Hata hivyo, Jaji Warioba aliliambia gazeti hili
jana kuwa hadi wanakutana juzi kwenye kikao cha mwisho cha tathmini
walikuwa hawajapokea barua ya kuvunjwa kwa tume yake.
“Barua ya Ikulu tumeipokea leo. Tulikuwa hatuna
taarifa kwamba tume yetu imevunjwa hadi tulipopokea barua leo (jana).
Tulifanya kikao chetu cha mwisho cha tathmini jana (juzi),” alisema
Warioba alipozungumza na Mwananchi jana jioni.
Warioba pia alithibitisha kwamba taarifa ya ufafanuzi (imechapishwa ukurasa wa 37) ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa hiyo ya Tume ya Warioba imetaja baadhi ya
sababu za kupendekezwa kwa muundo wa serikali tatu kuwa, ni pamoja na
Serikali ya Muungano kutokuwa tena na nguvu upande wa Zanzibar na Rais
kupokwa baadhi ya madaraka aliyopewa kikatiba.
Ufafanuzi wa Tume
Taarifa hiyo ya tume ilisema: “Waasisi walituachia
mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano. Katika
kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa
kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na
Katiba.”
Iliongeza: “Sehemu zote mbili ziliamua kuachia
baadhi ya mambo yake kuwa chini ya Serikali ya Muungano, sasa sehemu
moja inaondoa mambo yake. Kwa hiyo Serikali ya Muungano itakuwa
inashughulikia zaidi mambo ya upande mmoja.”
Kasoro nyingine iliyotajwa na tume hiyo ni hatua ya waasisi wa
Muungano kuwa waliacha Bunge lenye madaraka nchi nzima, lakini sasa ni
lazima sheria linazotunga zipate idhini ya Baraza la Wawakilishi kwa
upande wa Zanzibar.
“Waasisi waliacha Rais akiwa na madaraka kamili.
Madaraka hayo yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba. Waasisi
walituachia Mahakama ya Rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya
yamepunguzwa. Waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa moja. Sasa tunazo
nchi mbili,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Hii ndiyo inafanya wananchi wa Tanzania Bara
waamini Zanzibar ni huru katika mambo yao. Wanaona ina mamlaka kamili
kushughulikia mambo yake na imechukua rasilimali zake. S
erikali ya Muungano imebaki na mamlaka na rasilimali za Tanzania Bara.”
Taarifa hiyo ilisema wakati wabunge wa Zanzibar
wanashiriki kuamua mambo ya Tanzania Bara, wabunge wa Tanzania Bara
hawana nafasi ya kushiriki katika kuamua mambo ya Zanzibar.
Tume hiyo ilisema ilikuwa vigumu kwa Zanzibar
kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali, ikiwa ni pamoja na kufuta
kipengele cha nchi mbili kwenye Katiba yake, hivyo waliamua kupendekeza
mfumo wa serikali tatu kama hatua ya kuzingatia malalamiko ya Tanzania
Bara.
Tume iliona kwamba pamoja na mambo haya kufanywa
kinyume na Katiba ya Muungano, hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa
kufanya hivyo basi nayo yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza
Serikali ya Tanganyika iundwe.
Hali ilivyo
Tume hiyo imevunjwa huku kukiwa na mjadala mkali
kuhusu hotuba ya Jaji Warioba katika Bunge Maalumu pamoja na ile ya Rais
Kikwete aliyoitoa wakati akizindua Bunge hilo, Machi 21, mwaka huu.
Kutokana na hotuba hizo kukinzana, hasa kuhusu
aina ya muundo wa Muungano unaotakiwa, baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu walipendekeza Jaji Warioba apewe fursa ya kuitwa bungeni kutoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali na pengine kujibu baadhi ya hoja
zilizoibuliwa na Rais Kikwete.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu
wa kifungu cha 5 na 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kwa
Tangazo la Serikali Na.110 la 2012.
Wajumbe wake 30 waliteuliwa na Rais Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni